17 Juni 2026 - 14:41
Qalibaf: Vikosi vya Israel Vinapaswa Kujiondoa Kusini mwa Lebanon

Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, amesisitiza kuwa vikosi vya Israel vinapaswa kujiondoa kusini mwa Lebanon ili wananchi warejee makwao kwa heshima, huku Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih Berri, akiishukuru Iran kwa mchango wake katika juhudi za kusitisha vita.

Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (AS) –ABNA– Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, amesisitiza kuwa vikosi vya utawala wa Kizayuni vinapaswa kujiondoa mara moja kutoka kusini mwa Lebanon ili wananchi wa eneo hilo warejee katika nyumba na vijiji vyao kwa heshima na usalama.

Kwa mujibu wa IRNA, Qalibaf aliyasema hayo katika mazungumzo ya simu na Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih Berri, ambapo alieleza kuwa ushindi wa harakati za Muqawama ni mali ya Umma mzima wa Kiislamu na umetokana na damu na kujitolea kwa mashahidi.

Aidha, aliwakumbuka kwa heshima mashahidi wa Muqawama wa Hizbullah na Harakati ya Amal, hususan Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah (r.a.) na mashahidi wengine waliotoa maisha yao katika njia ya kuutetea Umma wa Kiislamu.

Qalibaf pia alisisitiza ulazima wa kusitishwa kwa vita katika maeneo yote, ikiwemo Lebanon, na akataka vikosi vya Israel viondoke katika maeneo yote vinayoyakalia ili wakazi wa kusini mwa Lebanon waweze kurejea nyumbani kwao kwa heshima na utulivu.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih Berri, aliishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa juhudi zake katika kufanikisha kusitishwa kwa vita nchini Lebanon, akimpongeza Qalibaf kwa mchango wake katika mazungumzo yaliyopelekea kupatikana kwa matokeo hayo.
Berri pia alitoa salamu za pole kwa mnasaba wa kuanza kwa mwezi mtukufu wa Muharram, akisisitiza kuwa roho ya Muqawama inapata nguvu kutokana na jihadi na mafundisho ya Imam Hussein (a.s.).

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha